Jiwe Maridadi
Jiwe Maridadi
NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI
Neno “moldavite” linakukumbusha nini? Watu wanaozungumza lugha nyingine wanaweza kufikiri kwamba ni kitu kinachopatikana katika Mto Moldau huko Ulaya ya Kati, ambao sasa unaitwa Mto Vltava. Au huenda ukafikiri ni jiwe adimu na maridadi. Basi, fasili hizo mbili zinafafanua vizuri neno moldavite.
Jiwe la moldavite ni kioo cha rangi ya kijani. Linapatikana kusini mwa Jamhuri ya Cheki, katika eneo lililo karibu na Mto Vltava. Jiwe hilo ni sehemu ya mawe yanayoitwa tektite—neno linalotokana na neno la Kigiriki tektos, linalomaanisha “kuyeyushwa,” au “hali ya kuyeyuka.” Kitabu Encyclopædia Britannica kinaeleza: “Mawe ya tektite yamechunguzwa sana na wanasayansi katika karne ya 20 kwa sababu inadhaniwa kwamba yanatoka nje ya dunia mahali pasipojulikana, lakini sasa imegunduliwa kwamba yanafanyizwa wakati miamba ya dunia inapoyeyuka na kugandamana haraka wakati vimondo vikubwa, nyota-mkia, au asteroidi zinapogonga uso wa Dunia.”
Mawe ya tektite yanapatikana katika mabara yote isipokuwa Antaktika na Amerika Kusini. Kwa kuwa moldavite yana chanzo cha pekee, huenda watu fulani wakafikiri kwamba mawe hayo yana nguvu za ajabu za angani na yanaweza kuponya. Hata hivyo, hayo ni mawe tu, ijapokuwa ni mawe maridadi sana yenye kuvutia.
Mawe hayo adimu yana rangi nyangavu sana ya kijani. Tofauti na mawe mengine ya tektite, mawe ya moldavite yanaweza kukatwa ili kutokeza vito maridadi. Wageni wanaotembelea Jamhuri ya Cheki wanaweza kuona mawe hayo kwenye sehemu ya vito katika Jumba la Makumbusho la Kitaifa huko Prague.
Biblia inatukumbusha hivi: “Dunia na vyote vinavyoijaza ni vya Yehova.” (Zaburi 24:1) Mawe yote yenye thamani ulimwenguni ni kati ya vitu hivyo vinavyoijaza dunia. Huenda ukakumbuka jambo hilo ukipata pendeleo la kuona jiwe maridadi la moldavite!
[Picha katika ukurasa wa 31]
“Moldavite” ambayo hayajasafishwa
[Picha katika ukurasa wa 31]
“Moldavite” lililokatwa
[Picha katika ukurasa wa 31]
Vito vya “moldavite”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Cut moldavite and bottom photos: Z knihy Svĕt drahých kamenů